Majaribio ya makombora ya Russia yamtia Obama mashakani
Russia imefanya majaribio ya makombora mapya suala ambalo limewatia wasiwasi viongozi na wanasiasa za Marekani. Inasemekana kuwa makombora hayo ni ya masafa ya kati.
Baada ya majaribio hayo maseneta kadhaa wa chama cha Republican wametoa taarifa wakikosoa siasa za nje za serikali ya Rais Barack Obama. Wanasema serikali ya Obama imeshindwa kuilazimisha Russia itekeleze majukumu na ahadi zake. Obama ambaye serikali yake haijaweza kutekeleza nara na kaulimbiu yake aliyotoa katika kampeni za uchaguzi wa Rais ya kufanya mabadiliko katika uhusiano wa Washington na Moscow, sasa anakabiliwa na changamoto mpya. Warepublican wa Marekani wanatumia hali hii ya sasa kukosoa mpango wa Obama wa kurekebisha uhusiano wa Russia ulipewa jina laReset . Kwa mujibu wa makubaliano ya pande mbili yaliyotiwa saini mwaka 1987 kati ya marais wa wakati huo wa Marekani na Russia Ronald Reagan na Mikhail Gorbachev, Washington na Moscow ziliahidi kuharibu makombora yao ya balestiki na Cruz yanayopiga umbali wa maili 300 hadi 3400. Makubaliano hayo pia yalisisitiza juu ya kusimamishwa uzalishaji na majaribio ya makombora hayo. Ni kwa kuzingatia hayo ndiyo maana Warepublican wanasisitiza kuwa majaribio ya sasa ya makombora mapya nchini Russia yanakiuka makubaliano hayo.
Marekani tayari imeliarifu shirika la kijeshi la NATO kuhusu majaribio hayo ya makombora mapya nchini Russia.
Makombora ya masafa ya kati ya Russia yanaweza kulenga maeneo ya kistratijia ya nchi za Ulaya.
Wachambuzi wa mambo wanasema kuwa iwapo viongozi wa Marekani watawasilisha malalamiko rasmi kwa Russia basi Washington itachukua hatua za kulipiza kisasi, suala ambalo litavuruga au kukwanisha mpango wa kuboresha uhusiano wa pande hizo mbili. Si hayo tu bali kwa sasa Obama anafanya mikakati ya kufunga mkataba mpya wa kistratijia na Russia katika uwanja wa kudhibiti silaha. Kufungwa mkataba huo kunahitaji uhusiano mwema na hali ya kuaminiana kati ya pande hizo mbili.
Ala kulli hal, taarifa iliyotolewa na viongozi wa chama cha Republican inaonesha kuwa chama hicho kinatumia suala la majaribio hayo ya silaha ya Russia kama wenzo wa kuishinikiza serikali ya Obama. Katika miaka ya hivi karibuni Warussia wamezidisha idadi ya makombora yao. Russia imechukua siasa hizo kama jibu la hatua ya Marekani ya kuweka makombora yake Ulaya mashariki hususan katika mipaka ya nchi waitifaki wake na Russia. Katika mkondo huo huo Moscow imetangaza kuwa, itaweka makombora yake ya balestiki ya Iskander katika eneo la Kaliningrad lililoko kaskazini mwa Poland kama kujibu hatua ya Washington ya kuweka mtambo wake wa makombora katika nchi hiyo.